Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), akiambatana na Dkt. Ali Taqavi, Rais wa Jamiat Al-Mustafa (s) nchini Tanzania, pamoja na Samahat Sayyid Arif Naqvi, walitembelea Hawzat Al-Qaim (as) iliyopo Tanga Mjini, Barabara ya 5.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Katika kuendeleza juhudi za kuimarisha elimu ya dini na mshikamano wa Kiislamu, viongozi mashuhuri wa taasisi mbalimbali za Kiislamu nchini Tanzania walifanya ziara maalum katika Hawzat Al-Qaim (as) iliyopo Tanga Mjini, Barabara ya 5.
Viongozi waliotembelea taasisi hiyo ni: Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), akiambatana na Dkt. Ali Taqavi, Mwakilishi wa Jamiat Al-Mustafa (s) nchini Tanzania, pamoja na Samahat Sayyid Arif Naqvi, Mkuu wa Taasisi ya Kiislamu ya Hojjat Asr Foundation Tanzania.
Katika hotuba yake kwa wanafunzi wa Hawza hiyo, Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum alisisitiza umuhimu wa elimu na maarifa katika kuendeleza Uislamu, akieleza kuwa maendeleo ya Uislamu hayawezi kupatikana bila Elimu na Maarifa, na bila Umoja miongoni mwa Waislamu.
Alibainisha kuwa umoja ni nguzo muhimu ya maelewano, maridhiano na amani ya kudumu, akihimiza ushirikiano baina ya madhehebu tofauti kwa ajili ya kuujenga Uislamu imara na wenye mafanikio.
Ziara hiyo ni ushahidi wa juhudi endelevu za kujenga maelewano ya kidini na kusaidia malezi ya viongozi wa baadaye wa Kiislamu kupitia Elimu ya Hawza.
Ziara hii muhimu ya viongozi hawa wa Kidini inabeba malengo haya yafuatayo:
1_Kuimarisha mahusiano ya kielimu na kiroho.
2_Kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kijamii na kidini.
3_Kuunga mkono juhudi za malezi ya kidini kwa vijana.
4_Kuonyesha mshikamano kati ya taasisi za kidini katika kanda hiyo.
Hawzat Al-Qaim (as) ni taasisi ya kidini inayotoa elimu ya juu ya Kiislamu, hasa kwa mujibu wa mafundisho ya Ahlul Bayt (as), na kuwepo kwa ziara ya Viongozi wa Kidini kama hii katika Hawzat hiyo ya Kielimu, ni ishara ya umuhimu wa taasisi hiyo katika muktadha wa Kiislamu nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Your Comment